Image courtesy of Amani Nation from Unsplash

“Mapenzi katika maisha ya mwanadamu ni kama mshipa upitishao damu mwilini ili kurutubisha kila sehemu ya mwili.”

Mengi yamesemwa kuhusu dondoo la mapenzi jijini Nairobi. Wengine wasingizia mapenzi Nairobi ni kitendawili kisicho teguka ilhali wengine wana msimamo penzi Nairobi lipo – na tena penzi dhabiti. Lakini wimbo “Nairobi” wake Bensoul waashiria taswira jipya. Hayawi hayawi huwa. Siku tuliokuwa tumeingoja kwa hamu na ghamu iliwadia tarehe 23/3/2020, mida ya saa kumi na mbili unusu. Wanachama wa Rotaract Club of Nairobi Central, waliandaa mkutano kwenye mtandao wa Zoom. Huu haukuwa mkutano wa kawaida kwani mkutano wa kawaida wanachama huwasiliana kwa njia ya kimombo. Lakini siku hii ilitengwa kama siku ya kukitukuza Kiswahili.

Ijapokuwa Kiswahili ni lugha ya taifa nchini, Wanachama na wageni walikuwa na siku mrefu kujieleza kupitia Kiswahili sanifu. Lo! Lugha iliyokuja kwa mashua ni kingereza ama Kiswahili? Kuwasiliana kwa Kiswahili kulionekana kuwa kizungumkuti kwa wanachama na wageni wengi, nikiwemo pia.

Tulianza na kuimba kitikio kwenye wimbo wa Nairobi tukiongozwa na msimamizi wetu. Mara ya mwisho uliimba na kujivinjari kwenye mkutano ni lini?

Msimamizi wetu Bi. Kamche alifungua mjadala kwa kuuliza swali. Mapenzi ni nini? Wanachama kadha wa kadha walitoa maoni yao kwa kusema; mapenzi ni kuvumiliana, kuelewana, kusameheana, kushirikiana, kusaidiana wakati wa dhiki na faraja na kuchagua kupenda kila siku. Wengine walikuwa na maoni tofauti – mengine ya ucheshi mengine ya kuvunja moyo.

Bi Kamche alitueleza kuwa mapenzi ni upendo mkubwa kwa mtu mwengine, sanasana hisia ya mvuto mkuu. Swala nyeti kwenye maelezo haya ni je, mtu huyo mwengine ana mvuto sawia kwako au wapenda pekee yako?

Haya basi. Mjadala uling’oa nanga kwa kuuliza je, unakubaliana na wimbo wa Bensoul? Nigependa kukujulisha kwanza wanachama wengi walikubaliana na wimbo huu huku wengine wakipinga abandan katan. Ikawa ni asilima nusu kwa nusu yaani 50/50 ilhali wengine wakabaki tikiti maji; hawajui waegemee mlengo upi. Wengine walisema mapenzi Nairobi ni mchezo wa bahati nasibu. Huku Nairobi ikiwa na sifa ya mji wa biashara, wanachama walisema mapenzi Nairobi ni sawa na shughuli za kibiashara.

Wahenga na wahenguzi hawakutupaka mafuta kwenye uti wa mgongo walipolonga na kunena ya kwamba, nidhamu njema zinawaelekeza binadamu wema kupenda binadamu wenzao. Sio kwa sababu ni matajiri au maskini bali kuwakubali wenzao. Waswahili husema mapenzi hayana macho wala maarifa lakini Nairobi…kunani?

Mapenzi Nairobi ni mikataba huru. Wahusika wanakutana na kujivinjari Pamoja – kisha wanaenda zao bila kuhusisha hisia zozote. Wanawake kwa waume wote wanashiriki ngono, hakuna uaminifu katika mahusiano yoyote.

Kizungumkuti kilichopigiwa debe na wanachama kadha ni wapenzi wa kanisa waliozama kwenye dini. Haswa wanaimbaji wa kwaya walionekana kutatanisha wapenzi wao kabisa. Wengi humlaumu shetani kwa kujaribu wana wa Mungu. Je, tumlaumu shetani ama tutamatishe kuwa wanachama wa kwaya ni hatari?

Uwezo wa kuwa na hela nyingi uwezavyo ni sawia moja na uwezo wako wa kupata mapenzi Nairobi. Hiki ni kizungumkuti kikuu hususan kwa wavulana wadogo wanaowatafuta wasichana iliw aasi ukapera. Fedha nazo Nairobi zimekuwa kigwezo. Warembo wamdhamini yule mwenye hela badala ya yule mwenye penzi! Nani atatuokoa kutoa pango hili?

Kuwepo kwa vipusa wengi na vijana wanaotaka kuchovya chovya asali pia ikawa ni kigezo katika mapenzi Nairobi. Mtaka yote hukosa yote. Vijana wachovya chovya wanaambulia patupu!

Bila shaka kunao wanachama waliotuelekeza kuwa kitendawili hiki cha mapenzi Nairobi kinaweza tatuliwa, kwani wamepata wachumba humu humu Nairobi. Lakini kukitega kitendawili hiki itabidi kila mmoja ajitume, anywe maji na amuombe Mola.

Mapenzi Nairobi yanachangamoto zake. Walakini, yule aliye na moyo safi na nia nzuri atapata penzi dhabiti kwani kila wingu jeusi lina utando. Mtaka cha uvunguni sharti ainame kwani utamu wa asali haupunguzi uchungu wa mvi wakenyuki Ungana nasi kwenye mkutano wetu ujao tarehe sita mwezi wa Aprili kutoka saa kumi na mbili jioni.

Makala haya yametayarishwa na; Rtr. Susan K. Maina

Katibu Msaidizi, RCNC 2020-2021.

Leave a comment